How To Know God - Kiswahili
UTIIFU WA KWELI MBELE ZA MUNGU
Kama Abraham alivyokuwa "rafiki Wa Mungu" kwa uvumilivu na
utiifu kwa Mungu, wewe pia unaweza kumjua Mungu na kupata rehema zake,
amani, na baraka. Kumjua Mungu kwa uvumilivu wa kweli katika kumwamini ni
ujuzi muhimu zaidi katika maisha. Ni ajabu namna gani kwamba Mungu
hujidhihirisha Mwenyewe kwa wote wanao Mtafuta kwa mioyo yao yote!
Ikiwa utageuka kuiacha njia yako na kweli kujitolea kwa Mungu, Roho Wake
ataishi ndani yako. Hakuna kitakacho kutenganisha na upendo Wake unapo
tumainia ahadi Zake na Kumfuata kwa utiifu. Yeye atakuwa Mungu wako, nawe
utakuwa hazina Yake Mwenyewe. Utagundua kwamba alikununua kwa gharama kuu,
na anataka kuwa na ushirika nawe—sasa na hata milele.
Uliza Mungu akupe ufahamu unapojifunza kurasa hizi za vifungu kutoka Neno
la Mungu. Mungu aliongoza watu wamchao kuandika maneno haya na kwa
kimiujiza ameyahifadhi katika vizazi vyote kutoka kwa majaribio yote ya
Shetani ya kuyakomesha.
______________________________________________________________
Maandiko yanayo husika katika kijitabu hiki yametolewa kutoka Biblia:
Sheria (Torah), Zaburi (Zabur), maandiko ya manabii, na Injili (Injil).
KUNA MUNGU WA KWELI MMOJA TU — 1
Kumbukumbu La Torati 6:4, 5
BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja. Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa
moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.
Isaya 45:18
Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye
aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa,
aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine.
1 Wafalme 8:60
Watu wote wa ulimwengu Wajue ya kuwa BWANA ndiye Mungu; hakuna mwingine.
Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu. —Isaya 42:8
Isaya 43:10, 11
Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA,. . . mpate kujua, na kuniamini, na
kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala
baada yangu mimi hatakuwapo mwingine. Mimi, naam, mimi, ni BWANA, zaidi
yangu mimi hapana mwokozi.
Isaya 45:22
Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni
Mungu; hapana mwingine.
MUNGU NI WA REHEMA NA NEEMA — 2
Zaburi 103:8, 11
BWANA amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, kadiri ileile rehema zake ni kuu
kwa Wamchao.
Zaburi 103:17, 18
Bali fadhili za BWANA zina Wamchao tangu milele hata milele,...maana, wale
walishikao agano lake, na kuyakumbuka maagizo yake ili wayafanye.
Mika 7:18
Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu,...kwa maana yeye
hufurahia rehema.
Maombolezo 3:22
Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, kwa kuwa rehema zake hazikomi.
Maombolezo 3:32
Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, kwa kadiri ya wingi wa huruma zake.
Zaburi 18:25
Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili.
1 Mambo Ya Nyakati 16:34
Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele.
MUNGU ANAKUPENDA — 3
Yeremia 31:3
BWANA alinitokea zamani, akisema, Naam, nimekupenda kwa upendo wa milele,
ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.
Yeremia 29:11
Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani,
wala Si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.
Malaki 1:2
Nimewapenda ninyi, asema BWANA.
Zaburi 103:13
Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo BWANA anavyowahurumia
wamchao.
Isaya 38:17
Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi kwa ajili ya amani yangu; Lakini kwa
kunipenda [ee Mungu] umeniokoa na shimo la uharibifu; kwa maana umezitupa
dhambi zangu zote nyuma yako.
1 Yohana 4:16, 19
Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Sisi
twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza.
Sefania 3:17
BWANA, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; atakushangilia
kwa furaha kuu, atatulia katika upendo wake. Atakufurahia kwa kuimba.
JAMBO KUBWA MUHIMU MAISHANI NI KUMJUA MUNGU — 4
Danieli 11:32
Lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu.
Yeremia 9:24
Bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na
kunijua, ya kuwa mimi ni BWANA, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika
nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema BWANA.
Kumbukumbu La Torati 30:19,
20
Nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana;
basi chagua uzima, kumpenda BWANA, Mungu wako, kuitii sauti yake na
kushikamana naye: kwani hiyo ndiyo uzima wako.
Zaburi 119:2
Heri wazitiio shuhuda zake, wamtafutao kwa moyo wote.
Zaburi 42:1
Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji. Vivyo hivyo nafsi yangu
inakuonea shauku, Ee Mungu.
Kutoka 33:14
Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.
KUJITEGEMEA PASIPO MUNGU NI KUANGAMIA — 5
2 Mambo Ya Nyakati 15:2
BWANA yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana
kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi.
Yeremia 17:9
Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani
awezaye kuujua?
Mithali 16:25
Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; lakini mwisho wake ni njia
za mauti.
2 Petro 2:4, 9
Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa
shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu. Basi,
Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika
hali ya adhabu hata siku ya hukumu.
1 Samweli 12:15
Bali msipoisikia sauti ya BWANA, mkiiasi amri ya BWANA, ndipo mkono wa
BWANA utakuwa juu yenu.
Yohana 15:6
Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu
huyakusanya na kuyatu. pa motoni yakateketea.
KUMJUA MUNGU NI LAZIMA TUMTAFUTE — 6
Yeremia 29:13
Nanyi mtanitafuta, na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.
Mithali 2:4, 5
Ukiutafuta kama fedha, . . . ndipo utakapo . . . pata kumjua Mungu.
Mathayo 7:7
Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi
mtafunguliwa.
Waebrania 11:6
Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu
lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa
thawabu wale wamtafutao.
Mithali 8:17
Nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.
Maombolezo 3:25
BWANA ni mwema kwa hao wamngojeao, kwa hiyo nafsi imtafutayo.
Matendo 17:26, 27
Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja. ...Ili wamtafute
Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na
kila mmoja wetu.
MUNGU ANATUTAKA TWENDE KWAKE — 7
2 Mambo Ya Nyakati 30:9
Kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ndiye mwenye neema, na mwenye rehema, wala
hatawageuzia mbali uso wake, mkimrudia.
Zaburi 86:5
Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, umekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa
fadhili, kwa watu wote wakuitao.
Yakobo 4:8
Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi.
Zaburi 145:18
BWANA yu karibu na wote Wamwitao, wote wamwitao kwa uaminifu.
Isaya 1:18
Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana,
zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa
kama sufu.
Mathayo 11:28, 29
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami
nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni
mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.
Yohana 6:37
Wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe.
MUNGU NI MTAKATIFU — 8
Kutoka 15:11
. . . Ni nani aliye kama wewe, Ee BWANA, . . . mtukufu katika utakatifu.
1 Samweli 2:2
Hakuna aliye mtakatifu kama BWANA; kwa maana hakuna ye yote ila wewe.
Ayubu 34:10
Mungu asidhaniwe kutenda udhalimu; wala Mwenyezi kuf anya uovu.
Isaya 6:3
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa
utukufu wake.
Isaya 57:15
Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni
Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu.
Zaburi 145:17
BWANA ni mwenye haki katika njia zake zote, na mwenye fadhili juu ya kazi
zake zote.
Marko 10:18
Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.
Ufunuo 15:4
Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? kwa kuwa wewe peke
yako u Mtakatifu.
WATU WA MUNGU NI LAZIMA WAISHI MAISHA MATAKATIFU — 9
Yakobo 2:19, 20
Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini
na kutetemeka. Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba
imani pasipo matendo haizai?
1 Yohana 2:4; 3:10
Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli
haimo ndani yake. Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa
Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye
asiyempenda ndugu yake.
Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA; bali humpenda mtu afuatiaye wema. —Mithali 15:9
Waebrania 12:14
Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao
hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao.
Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. —1 Petro 1:15
Amosi 5:14
Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi; hivyo BWANA, Mungu wa
majeshi, atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo.
MAMBO MUNGU ANAYOAMURU — 10
Mika 6:8
Na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na
kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!
Mambo Ya Walawi 19:2
Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu
wenu, ni mtakatifu.
Luka 10:27
Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na
kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani
yako kama nafsi yako.
Marko 10:19
Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie
uongo, Usi danganye, Waheshimu baba yako na mama yako.
Warumi 12:2
Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali
mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu.
Yoshua 1:8
Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako,
bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa
na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako,
kisha ndipo utakapositawi sana.
Marko 11:22
Mwaminini Mungu.
MAMBO MUNGU ANAYOCHUKIA — 11
Mithali 6:16-19
Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA; naam, viko
saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, na mikono imwagayo
damu isiyo na hatia; moyo uwazao mawazo mabaya; miguu iliyo myepesi kukimbilia
maovu; shahidi wa uongo asemaye uongo; naye apandaye mbegu za fitina kati ya
ndugu.
Isaya 61:8
Maana mimi, BWANA, naipenda hukumu ya haki,
nauchukia wivi na uovu.
Ufunuo 21:8
Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na
wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na
waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo
mauti ya pili.
Malaki 2:15, 16
Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote
asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. Maana mimi nakuchukia kuachana,
asema BWANA.
Zekaria 8:17
Wala mtu wa kwenu asiwaze mabaya moyoni mwake juu
ya jirani yake; wala msipende kiapo cha uongo; maana hayo yote ndiyo
niyachukiayo, asema BWANA.
WATU HUPUNGUKIWA NA MATAKWA YA MUNGU — 12
Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. —Yohana 5:42
Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote. —Yakobo 2:10
Isaya 6:5
Ndipo niliposema, Ole wangu! kwa maana nimepotea;
kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye
midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA wa majeshi.
Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi. —Yakobo 4:17
Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, hakuna mwenye haki hata mmoja. —Warumi 3:10
Warumi 3:23
Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa
na utukufu wa Mungu.
1 Yohana 3:10
Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu,
wala yeye asiyempenda ndugu yake.
Isaya 53:6
Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu
amegeukia njia yake mwenyewe.
Ni nani awezaye kusimama mbele za BWANA, huyu Mungu mtakatifu? —1 Samweli 6:20
KAZI ZETU WENYEWE HAZIWEZI KUMPENDEZA MUNGU — 13
Warumi 10:2, 3
Kwa maana nawashuhudia kwamba wana
juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa. Kwa maana, wakiwa hawaijui
haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya
haki ya Mungu.
Isaya 64:6
Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye
mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi.
Ezekieli 33:13
Nimwambiapo mwenye haki, ya kwamba hakika
ataishi; kama akiitumainia haki yake, akatenda uovu, basi
katika matendo yake ya haki, hata mojawapo halitakumbukwa; bali katika uovu wake
alioutenda, atakufa katika uovu huo.
Warumi 8:8; 3:20
Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.
Kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya
sheria.
2 Wakorintho 3:5
Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo
lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu.
DHAMBI HUTUTENGANISHA NA MUNGU — 14
Warumi 5:12
Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia
ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa
sababu wote wamefanya dhambi.
Yakobo 1:15
Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa
dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.
Ezekieli 18:20
Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa.
Isaya 59:2
Lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu
wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata
hataki kusikia.
Mithali 11:19
Haki huelekea uzima; afuataye maovu hufuata mauti
yake mwenyewe.
2 Mambo Ya Nyakati 24:20
Mungu asema hivi, Kwani ninyi kuzihalifu amri za
BWANA, hata msiweze kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha BWANA, yeye naye amewaacha
ninyi.
1 Samweli 15:23
Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, na ukaidi
ni kama ukafiri na vinyago; kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, yeye naye
amekukataa wewe.
GHADHABU YA MUNGU JUU YA DHAMBI — 15
Zaburi 7:11
Mungu ni mwamuzi mwenye haki, naam, Mungu
aghadhibikaye kila siku.
Nahumu 1:3
BWANA si mwepesi wa hasira, ana uweza mwingi,
wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe.
Wakolosai 3:6
Kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu.
Warumi 1:18
Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka
mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu.
Warumi 1:29-32
Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa
na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya,
wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye
kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio
na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; ambao
wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili
mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.
HUKUMU IKO MBELE — 16
Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu. —Waebrania 9:27
Ufunuo 20:12, 15
Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama
mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine
kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo
yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Na iwapo mtu ye yote
hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la
moto.
Waebrania 10:31
Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai.
Mathayo 12:36
Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana,
watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu.
Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la sir likiwa jema au likiwa baya. —Mhubiri 12:14
Mathayo 13:49, 50
Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia;
malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika
tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
HATUWEZI KUJIFICHA KUTOKANA NA MUNGU — 17
Mithali 15:3
Macho ya BWANA yako kila mahali; yakimchunguza
mbaya na mwema.
Zaburi 139:1-4
Ee BWANA, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua
kuketi kwangu na kuondoka kwangu; umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta
kwenda kwangu na kulala kwangu, umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno
ulimini mwangu usilolijua kabisa, BWANA.
1 Samweli 16:7
Kwakuwa BWANA haangalii kama binadamu
aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA
huutazama moyo.
Zaburi 94:9
Aliyelitia sikio mahali pake asisikie?
Aliyelifanya jicho asione?
Yeremia 16:17
Maana macho yangu yaziangalia njia zao zote;
hawakufichwa uso wangu usiwaone, wala haukusitirika uovu wao macho yangu
yasiuone.
Waebrania 4:13
Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake,
lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.
KUGEUKA NA KUTOKA DHAMBINI KUNAHITAJIKA — 18
Ezekieli 18:23
Je! mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? asema
Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?
Luka 13:3
Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote
mtaangamia vivyo hivyo.
Mithali 28:13
Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye
aziungamaye na kuziacha atapata rehema.
Yoeli 2:12, 13
Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa
mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu,
wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye
neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.
Hosea 14:2
Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie BWANA;
mkamwambie, Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema.
Ayubu 33:27, 28
Yeye huimba mbele ya watu, na kusema, mimi
nimefanya dhambi, yeye ameikomboa nafsi yangu isiende shimoni, an
uhai wangu utautazama mwanga.
KUTUBU KUNALETA MSAMAHA — 19
Isaya 55:6, 7
Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, mwiteni, maadamu yu karibu; mtu
mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki aache mawazo yake; na amrudie BWANA,
naye atamrehemu; na arejee kwa Mungu wetu, naye atamsamehe kabisa.
Zaburi 34:18
BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo, na
waliopondeka roho huwaokoa.
Yeremia 36:3
Wapate kurudi, kila mtu akaiache njia yake mbaya;
nami nikawasamehe. . . dhambi yao.
Zaburi 32:5
Nalikujulisha dhambi yangu, wala sikuuficha
upotovu wangu. Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa BWANA, nawe ukanisamehe
upotovu wa dhambi yangu.
1 Yohana 1:9
Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa
haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.
Matendo 3:19
Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe.
Kutubu kunamaanisha kugeuka kutoka dhambini pamoja na kuungama mbele za Mungu.
DHABIHU INAYOTAKIKANA KUTUPATANISHA NA MUNGU — 20
(Dhambi ilileta utengano.)
Mambo Ya Walawi 17:11
Kwa kuwa uhai
wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili
kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo
upatanisho kwa sababu ya nafsi.
Waebrania 9:22
Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na
pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo
Kutoka 12:5, 13
Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja. ...Na ile damu itakuwa ishara kwenu
katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu,
lisiwapate pigo lo lote likawaharibu.
Mwanzo 22:8, 13
Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia
mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. . . . Ibrahimu akainua macho yake,
akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika
kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya
kuteketezwa badala ya mwanawe.
YESU NDIYE MWANA KONDOO ALIYETOLEWA NA MUNGU — 21
Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! —Yohana 1:29
Alionewa, lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake; kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatao manyoya yake; naam, hakufunua kinywa chake. —Isaya 53:7
Wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa
damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata
ukombozi wa milele. Kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja
azichukue dhambi za watu wengi. . . . Basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye
kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na
mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye
hai? —Waebrania 9:12,28, 14
1 Petro 1:18, 19
Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu
viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo
asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.
UKOMBOZI NI KWA MAAFIKANO TU NA MUNGU — 22
Warumi 3:24, 25
Wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa
njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe
upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake.
Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. —Warumi 5:8,9
Hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu. —Wagalatia 2:16
Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. —Waefeso 2:8,9
Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa
jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi. —Matendo 10:43
Matendo 4:12
Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote,
kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo
sisi kuokolewa kwalo.
KUZALIWA KWA YESU KWATANGAZWA — 23
Luka 1:26-38
...Malaika Gabrieli alitumwa na Mungu
kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira
aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake
bikira huyo ni Mariamu. ...Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana
umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na
jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, ...na
ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu
akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu
zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa
kitakatifu, Mwana wa Mungu.... kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.
Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama
ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
Watu tu walioingia Ulimwenguni pasipo uzao wa Mume na Mke walikuwa Adamu na Kristo. Adamu alileta dhambi katika Ulimwengu, lakini Yesu alileta ushindi juu ya dhambi.
KWA KWELI YESU NI NANI — 24
Wafilipi 2:6, 8
Ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya
Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;
tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata
mauti, naam, mauti ya msalaba.
Yohana 10:30, 36
Mimi na Baba tu umoja. Je! yeye ambaye Baba
alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu
nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu?
Yesu Kristo, Neno la Milele, amekuwako
daima. Kwa muujiza, Mungu alisababisha atungwe mimba katika tumbo la Mariamu.
Kimwili anajulikana kama Mwana wa Mtu, na Kiroho anajulikana kama Mwana wa
Mungu. Maandiko yanatumia neno "Mwana" kueleza uhusiano ulioko kati ya
Mungu na Neno lake—Yesu Kristo.
Waebrania 10:5
Kwa hiyo ajapo . . . Lakini mwili uliniwekea
tayari.
Na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa
Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana
wetu. —Warumi 1:4
Yohane 20:28
Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na
Mungu wangu!
KWA KWELI YESU NI NANI — 25
1 Timotheo 3:16
Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu
alidhihirishwa katika mwili.
Wakolosai 2:9
Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa
Mungu, kwa jinsi ya kimwili.
Isaya 9:6
Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa
mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina
lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.
Yohana 8:58
Yesu akawaambia, . . . Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.
Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu
ulipata kuwako, wala ulimwengu haukum tambua. —Yohana 1:10
1 Timotheo 2:5, 6
Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati
ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe
kuwa ukombozi kwa ajili ya wote.
Wakolosai 1:14, 15
Ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani,
msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana.
BIBLIA (MAANDIKO) NI NENO LA MUNGU — 26
Maana unabii haukuletwa po pote kwa
mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa
na Roho Mtakatifu. —2 Petro 1:21
Luka 1:70, 77
Kama alivyosema tangu mwanzo kwa kinywa cha
manabii wake watakatifu; uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi
zao.
Roho ya BWANA ilinena ndani yangu, na neno lake likawa ulimini mwangu. —2 Samweli 23:2
Kumbukumbu La Torati 6:6
Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa
katika moyo wako.
2 Timotheo 3:16
Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa
mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa
kuwaadibisha katika haki.
Warumi 15:4
Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa
yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate
kuwa na tumaini.
Mathayo 22:29
Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala
uweza wa Mungu.
Zaburi 138:2
Kwa maana umeikuza ahadi yako, kuliko jina
lako lote.
YESU NDIYE NENO LA MUNGU — 27
Ufunuo 19:13
Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu,
na jina lake aitwa, Neno la Mungu.
Yohana 1:1, 14
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno
alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa
kwetu.
Yesu anamdhihirisha Mungu
2 Wakorintho 4:6
Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang’aa
toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa
Mungu katika uso wa Yesu Kristo.
Yohana 1:18
Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote;
Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.
Mungu yuanena kuptia kwa Yesu
Waebrania 1:1, 2
Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu
katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema
na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya
ulimwengu.
Yohana 8:38
Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo.
NENO LILILOANDIKWA NA LILILO NA UHAI KU LINGAN ISHWA — 28,29
Biblia ni chakula kwa nafsi
Ayubu 23:12
Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu.
Mathayo 4:4
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika
kinywa cha Mungu.
Biblia inaangaza njia yetu
Zaburi 119:105
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, na kumfahamisha mjinga. —Zaburi 119:130
Yesu ni mkate kutoka mbinguni
Yohana 6:51, 48
Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka
kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa
mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Mimi ndimi chakula cha
uzima.
Yesu ni nuru ya ulimwengu
Yohana 8:12
Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi
nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru
ya uzima.
Biblia huleta maisha yen ye
mazao
Zaburi 1:2, 3
Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, na
sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
kandokando ya vijito vya maji, uzaao matunda yake kwa majira yake, wala jani
lake halinyauki; na kila alitendalo litafanikiwa.
Yesu hutoa maisha yen ye mazao
Yohana 15:4a, 5
Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Mimi ni
mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana;
maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.
MAANDIKO YAELEZA JUU YA YESU KRISTO
Yohana 5:39, 46
Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani
kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. . .
. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu.
Luka 24:27
Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika
maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.
NENO LA MUNGU LA MILELE HALIBADILIKI — 30
Zaburi 119:89, 160
Ee BWANA, neno lako lasimama imara mbinguni
hata milele. Jumla ya neno lako ni kweli, na kila hukumu ya haki yako ni ya
milele.
Isaya 40:8
Majani yakauka, ua lanyauka; bali neno la Mungu wetu
litasimama milele.
Mathayo 5:18
Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja
ya torati haitaondoka, hata yote yatimie.
Yohana 10:35
Na maandiko hayawezi kutanguka.
Mtu asijaribu kubadilisha maneno ya Biblia
Kumbukumbu La Torati 12:32
Neno niwaagizalo lo lote liangalieni kulifanya; usiliongeze,
wala usilipunguze.
Mithali 30:6
Usiongeze neno katika maneno yake; asije akakulaumu,
ukaonekana u mwongo.
Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima. —Ufunuo 22:19
Mithali 13:13a
Kila alidharauye neno hujiletea uharibifu.
KIFO CHA YESU KILIKAMILISHA MPANGO WA MUNGU — 31
Yohana 10:17, 18
Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai
wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami
ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena.
Mathayo 26:53, 54
Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba
yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?
Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?
Matendo 3:18
Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake
wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo.
Matendo 2:23
Mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu
lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulibisha kwa mikono
ya watu wabaya, mkamwua.
Isaya 53:10
Lakini BWANA aliridhika kumchubua;
amemhuzunisha; utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi.
KIFO CHA YESU KUTANGAZWA NA MASHAHIDI — 32
Marko 15:27, 28
Na pamoja naye walisulibisha wanyang’anyi
wawili, mmoja mkono wake wa kuume na mmoja mkono wake wa kushoto. Basi andiko
likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.
Mathayo 27:45, 50-51, 54
Basi tangu saa sita palikuwa na giza
juu ya nchi yote hata saa tisa. . . . Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa
nguvu, akaitoa roho yake. . . . nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka. Basi yule
akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la
nchi na mambo ya liyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika
huyu alikuwa Mwana wa Mungu.
Yohana 19:32-37
Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa
kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona
ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; lakini askari mmojawapo alimchoma
ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. ...Kwa maana hayo yalitukia
ili andiko litimie, hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na...watamtazama yeye
waliyemchoma.
YESU ALISHINDA KIFO — 33
Matendo 2:24, 32
Ambaye Mungu alimfufua, akiufungua uchungu wa
mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao. Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi
sote tu mashahidi wake.
Waebrania 2:14, 15
Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na
mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti
amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale
ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.
1 Wakorintho 15:55, 57
Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi,
Ewe mauti, uchungu wako? Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana
wetu Yesu Kristo.
Ufunuo 1:18
Na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na
tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.
2 Timotheo 1:10
Na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake
Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na
kutokuharibika, kwa ile Injili.
YATUPASA TUFANYEJE NA YESU? — 34
Ufunuo 3:20
Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu
akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula
pamoja naye, na yeye pamoja nami.
Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauWa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki. —Warumi 4:5
Yohana 20:22; 16:24
Pokeeni Roho Mtakatifu...ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe
timilifu.
Warumi 10:9
Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya
kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu
alimfufua katika wafu, utaokoka.
Mathayo 10:37, 16:24, 25
Apendaye baba au mama kuliko mimi,
hanistahili; ...Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka
kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu
atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa
ajili yangu, ataiona.
Wagalatia 3:29
Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao
wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.
KUPITIA KWA YESU TUNA UZIMA MPYA — 35
1 Yohana 5:11, 12
Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa
uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao
huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima.
Wagalatia 2:20
Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini
ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao
sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu.
Warumi 8:2
Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio
katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na
mauti.
2 Wakorintho 5:17
Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo
amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! yamekuwa mapya.
1 Petro 1:23; 2:2
Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu
iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo
hata milele. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili
yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu.
MUNGU NI BABA KWA WATU WAKE — 36
Zaburi 68:5
Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu
katika kao lake takatifu.
Isaya 64:8, 63:16
Lakini sasa, Ee BWANA, wewe u baba yetu; sisi
tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako. Wewe, BWANA,
ndiwe Baba yetu, mkombozi wetu tangu milele ndilo jina lako.
Hosea 1:10
Tena itakuwa, badala ya kuambiwa, Ninyi si
watu wangu, wataambiwa, Ninyi ndio wana wa Mungu aliye hai.
Mathayo 7:11; 6:9
Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa
watoto wenu vipawa vyema, je! si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa
mema wao wamwombao?. . . Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina
lako litukuzwe, Ufalme wako uje.
2 Wakorintho 6:17b, 18
Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu,
nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike.
Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. —Warumi 8:14
KUPITIA KWA YESU TUNAMJUA MUNGU KAMA BABA — 37
Yohana 14:6, 7, 23
Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na
uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi,
mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Mtu akinipenda,
atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya
makao kwake.
Wagalatia 4:4-7; 3:26
...Mungu alimtuma Mwanawe...ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.
Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu ali mtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni
hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa
Mungu. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika
Kristo Yesu.
Yohana 1:12
Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa
kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.
1 Yohana 2:1
Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi
kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki.
YESU HULETA UPENDO, FURAHA, AMANI — 38
1 Yohana 4:16
Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo,
hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.
Waefeso 4:32
Tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye
huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.
Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi
mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi. —Yohana 13:35
Wagalatia 5:22
Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha,
amani...
Walakini nitamfurahia BWANA, nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu. —Habakuki
3:18
Zaburi 16:11
Utanijulisha njia ya uzima; mbele za uso wako
ziko furaha tele; na katika mkono wako wa kuume mna mema ya milele.
Warumi 5:1
Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika
imani, na tuwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Yohana 14:27
Amani nawaachieni; amani yangu nawapa;
niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala
msiwe na woga.
YESU ATAWAFUFUA WAFUASI WAKE WA KWELI — 39
Warumi 8:11
Lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye
aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali
ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.
1 Wakorintho 6:14
Naye Mungu alimfufua Bwana, na tena atatufufua sisi kwa uweza
wake.
Yohana 11:25, 26
Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye
aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini
hatakufa kabisa hata milele.
1 Wakorintho 15:21-23
Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu,
kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote
wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. Lakini kila mmoja mahali
pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja.
Yohana 14:19
Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa
hai.
USIDHARAU WOKOVU HUU MKUU — 40
Waebrania 10:28, 29
Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo
huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu. Mwaonaje? Haikumpasa adhabu
iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya
agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?
Yohana 12:48
Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno
yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya
mwisho.
Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu
msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakuf a katika dhambi zenu. —Yohana 8:24
Luka 12:4, 5
Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope
hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi. Lakini
nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa
kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo.
Waebrania 2:3
Sisi je! tutapataje kupona, tusipojali wokovu
mkuu namna hii?
YESU KRISTO ATATUHUKUMU — 41
Matendo 17:31
Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu
walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti
wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.
Yohana 5:22, 23
Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa
Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu
Baba.
2 Wakorintho 5:10
Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa
mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee. kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au
mabaya.
Warumi 2:16
Katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za
wanadamu, kwa Kristo Yesu.
2 Wathesalonike 1:7, 8
Wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka
mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake; katika mwali wa moto; huku akiwalipiza
kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu.
Luka 19:27
Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale,
waleteni hapa mwachinje mbele yangu.
SIO WOTE WANAOSHUHUDIA KUMFUATA YESU WALIO WA
YESU — 42
Tito 1:16
Wanakiri ya kwamba wanamjua Mungu, bali kwa
matendo yao wanamkana.
Warumi 8:9
Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa
Kristo, huyo si wake.
Ezekieli 33:31
Nao hukaa mbele yako kama watu wangu, nao
husikia maneno yako, wasiyatende; maana kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye
upendo mwingi, lakini mioyo yao inatafuta faida yao.
Mathayo 15:8
Watu hawa huniheshimu kwa midomo; ila mioyo
yao iko mbali nami.
Mathayo 7:21-23
Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana,
atakayeingia katika uf alme wa mbinguni; bali ni yeye af anyaye mapenzi ya Baba
yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya
unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya
miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni
kwangu, ninyi mtendao maovu.
WAFUASI HALISI WA YESU HUMII
— 43
1 Yohana 2:3
Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika
amri zake.
Ezekieli 36:27
Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika
sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.
Waebrania 5:9
Naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa
milele kwa watu wote wanaomtii.
Warumi 6:18
Na mlipokwisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mkawa watumwa wa
haki.
Waefeso 2:10
Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo
Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende
nayo.
Warumi 8:10, 13
Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa
kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki. Kwa maana kama
mkiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo
ya mwili kwa Roho, mtaishi.
2 Timotheo 2:19
Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.
ULIMWENGU UNACHUKIA WAFUASI WA YESU — 44
Yohana 15:18, 19
Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa
umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu,
ulimwengu ungewapenda walio wake, lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali
mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.
Yohana 16:2, 3
Naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye
ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba
wala mimi.
1 Yohana 3:1
Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa
Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa
haukumtambua yeye.
Matendo 14:22
Na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme
wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.
2 Timotheo 3:12
Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa
katika Kristo Yesu wataudhiwa.
Yohana 16:33
Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo;
mimi nimeushinda ulimwengu.
AHADI KWA WANAO DHULUMIWA — 45
Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa
maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. —1 Petro 5:7
Isaya 41:10
Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe;
usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia,
naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.
Baba yangu na mama yangu wameniacha, bali
BWANA atanikaribisha kwake. —Zaburi 27:10
Waebrania 13:6
Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye
anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?
1 Petro 4:14
Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri
yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.
Zaburi 91:11; 23:4
Kwa kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde
katika njia zako zote. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja nami.
Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. —Wafilipi 4:13, 19
USHINDI JUU YA DHAMBI NA SHETANI — 46
1 Wakorintho 10:13
Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo
kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita
mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze
kustahimili.
Waebrania 4:16
Basi na tukikaribie kiti cha flee-ma kwa
ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
2 Timotheo 2:22
Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate
haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo
safi.
1 Yohana 1:7
Bali tukienenda nuruni, kama yeye ahivyo
katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake,
yatusafisha dhambi yote.
Warumi 6:11
Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu
kwa dhambi, na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.
Yakobo 4:7
Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye
atawakimbia.
Zaburi 119:11
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije
nikakutenda dhambi.
MAOMBI YA KWELI NI USHIRIKA NA MUNGU — 47
Zaburi 27:8
Uliposema, Nitafuteni uso Wangu, Moyo wangu
umekuambia, BWANA, uso wako nitautafuta.
Zaburi 62:8
Enyi watu, mtumainini sikuzote, ifunueni mioyo
yenu mbele zake; Mungu ndiye kimbilio letu.
Yeremia 17:14
Uniponye, Ee BWANA, nami nitaponyeka; uniokoe,
nami nitaokoka; kwa maana wewe ndiwe uliye sifa zangu.
1 Wathesalonike 5:17, 18
Ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo;
maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.
Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. —Yakobo 1:5
Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu
yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. —Yohana 15:7
Zaburi 34:4
Nalimtafuta BWANA akanijibu, akaniponya na
hofu zangu zote.
Zaburi 66:18; 25:11
Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, Bwana
asingesikia. Ee BWANA, kwa ajili ya jina lako, unisamehe uovu wangu, maana ni
mwingi.
YESU ANAKUJA—UWE TAYARI! — 48
1 Wathesalonike 4:16, 17
Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka
mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao
waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia,
tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo
tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo.
2 Wakorintho 7:1
Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo,
na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza
utakatifu katika kumcha Mungu.
1 Yohana 2:28
Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili
kusudi, atakapofunuliwa, tuwe na ujasiri, wala tusiaibike mbele zake katika kuja
kwake.
Yakobo 5:8, 9
Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa
maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu, msinung’unikiane msije mkahukumiwa.
Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango.
Luka 12:40
Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani
ndipo ajapo Mwana wa Adamu.
UJAZWE NA ROHO WA MUNGU
Mithali 1:23
Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu; tazama, nitawamwagia roho yangu, na
kuwajulisheni maneno yangu.
Matendo 2:38
Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la
dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Waefeso 5:18-21
Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana
kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia
Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote,
katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo; hali mnanyenyekeana katika kicho
cha Kristo.
Wafilipi 2:13
Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda
kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.
1 Wakorintho 3:16; 6:2
Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu
anakaa ndani yenu? Maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni
Mungu katika miili yenu.
Text from Bible in Kiswahili, United Bible Societies, Africa Regional Centre, ©1952. Used by permission.
If you are interested in receiving additional studies of God’s
Word, write to the publisher or order online:
W.M. Press, Inc.
P.O. Box 120
New Paris, Indiana 46553 U.S.A.
Bure — Hakiuzwi
1515 Kiswahili
World Missionary Press Home Page | Go to the Top of This Page